Serikali ya Tanzania yathibitisha dhamira yake ya kuunga mkono watetezi wa haki za binadamu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, amesisitiza kwamba serikali inatambua umuhimu wa watetezi wa haki za binadamu na inaendelea kuchukua hatua zinazofaa ili kuwapatia ulinzi wa kisheria. Kauli hii ilitolewa wakati wa mafunzo ya wanachama wapya wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, THRDC.
Maswi alifafanua kwamba wizara yake imepokea Sera ya Mfano ya Watetezi wa Haki za Binadamu ambayo imeandaliwa na THRDC, na sasa ipo katika hatua za kuingizwa rasmi kwenye mfumo wa serikali. “Tunaendelea kujadiliana na THRDC ili kuona uwezekano wa kuidhinisha sera hii au kuiboresha zaidi, kwa lengo la kuwa sera rasmi ya serikali na kuwezesha utungwaji wa sheria maalum kwa ajili ya watetezi wa haki za binadamu,” aliongeza Maswi.
Amesisitiza pia kwamba serikali inathamini mchango muhimu wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika kulinda haki za binadamu na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.
Kati ya changamoto zilizozungumziwa, Maswi alitaja ukosefu wa sheria maalum za kuwalinda watetezi wa haki za binadamu. Alisema serikali iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali kupokea mapendekezo ya maboresho ya sheria ili kuboresha hali ya kazi za mashirika yasiyo ya kiserikali.
Maswi alisisitiza pia kuwa serikali ina mpango wa kuingiza elimu ya haki za binadamu katika mtaala wa shule na vyuo, kama njia ya kupunguza matukio ya ukiukwaji wa haki hizo nchini.
Kwa upande wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), Rais wake, Wakili Boniface Mwabukusi, alisisitiza kwamba utetezi wa haki za binadamu ni kazi ya wito inayohitaji kujitolea kwani watetezi hawa ni sauti kwa wasio na sauti.
Mratibu kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, aliwashauri wanachama wapya wa mtandao huo kutekeleza majukumu yao kwa kufuata miongozo, kanuni na sheria za nchi.
Mafunzo ya siku mbili yaliwaleta pamoja wanachama wapya wa THRDC kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali 53, yakilenga kuwajengea uwezo katika kutetea haki za binadamu na kushirikiana na serikali katika ajenda hiyo. THRDC kwa sasa ina wanachama zaidi ya 300 wanaofanya kazi nchini Tanzania Bara na visiwani.