Watu wawili wameaga dunia katika ajali ya gari iliyohusisha Toyota Noah kuigonga Toyota Canter, usiku wa kuamkia leo katika eneo la Kauzeni, Kata ya Kwenjugo, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amesema kwamba Noah ilikuwa ikitoka barabara ya Korogwe kuelekea Handeni, na ilipofika kwenye kona ya Kauzeni, dereva alishindwa kuimudu na kugonga Canter iliyokuwa pembeni ya barabara.
Abiria kadhaa waliokuwa ndani ya Noah walipata majeraha na walikimbizwa Hospitali ya Mji Handeni. Miili ya marehemu imehifadhiwa ili kufanyika taratibu nyingine.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando, alithibitisha kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma kwamba miongoni mwa waliofariki ni askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kutoka Kikosi cha 83 Vigwaza, aliyefahamika kwa jina la Abdul Kareem Kimemeneke, mwenye umri wa miaka 49 na mkazi wa Kwamfuko, Kata ya Vibaoni, Handeni.