Wafugaji kuku wa nyama wanashauriwa kuepuka matumizi ya dawa za antibayotiki, ambazo sasa zinaongeza usugu wa vimelea dhidi ya dawa mwilini.
Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa watu milioni 1.2 hufariki kila mwaka kutokana na usugu wa vimelea, huku ikiashiriwa kwamba ifikapo mwaka 2030, idadi hii inaweza kufikia milioni 10.
Katika mahafali ya wafugaji wa Kata ya Chanika waliofunzwa ufugaji wa kuku wa nyama bila dawa, Daktari wa Mifugo amesema lengo ni kuepusha usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
“Wafugaji wote wanashauriwa kutumia wataalam ili kufuga kwa ubora na kupunguza matumizi ya dawa, iwe kwa samaki, kuku, au mifugo mingine. Dawa zitumike tu pale inapohitajika, na wanaposhuhudia mifugo ikiona dalili za ugonjwa, wawatafute wataalam,” amesema Daktari huyo.
Amesema mradi huo unalenga kupunguza matumizi ya dawa kwa kuhamasisha wafugaji kutumia chanjo na kuzingatia usafi wa mabanda na vyakula vya mifugo.
Mafunzo yamejikita kwenye ufugaji wa kuku kwa kuwa hutoa protini kwa haraka zaidi ikilinganishwa na mifugo mingine kama vile ng’ombe na mbuzi.
Utafiti uliofanywa umeonyesha kuwa bila jitihada zaidi, kutakuwa na upungufu wa protini inayohitajika katika siku zijazo.
Daktari huyo alionya kuwa wafugaji wengi hawana elimu sahihi, jambo ambalo limewafanya kugeukia dawa badala ya chanjo, hali ambayo inaongeza usugu wa vimelea.
“Mdudu akiota usugu akiwa kwa mnyama anaweza kuhamishwa kwa binadamu, na hivyo usugu unaendelea. Binadamu akitibiwa kwa dawa, hatapata matokeo mazuri,” alisema.
Mratibu wa mradi huo amesema watu hupata usugu wa vimelea kwa kula mazao ya mifugo au shambani ambayo yana masalia ya dawa zilizotumika. Amesisitiza kuwa changamoto ya usugu wa vimelea inaleta vifo vingi zaidi kuliko magonjwa mengine.
Mafunzo hayo yamefanyika katika halmashauri sita nchini, na yana lengo la kuongeza uelewa kuhusu usugu wa vimelea kwa wafugaji. Mradi umeanzishwa ili kukabiliana na changamoto za usugu wa vimelea dhidi ya dawa, hasa miongoni mwa kuku wa nyama.
Wafugaji wengi wanaamini kuwa kuku lazima wapewe dawa, jambo linalosababisha matumizi yasiyo ya lazima ya dawa. Mradi unakusudia kuboresha mbinu za ufugaji zinazowezesha kuku kukua bila magonjwa, hivyo kupunguza shinikizo la matumizi ya dawa.
Kuku wanaozalishwa kwa mfumo huu wana uzito wa zaidi ya kilo mbili, na kupitia mradi huo, wameweza kuuzwa kwa bei ya juu kutokana na afya zao bora na ladha nzuri.
Mmoja wa wafugaji kutoka Kata ya Chanika amesema; “Mwanzoni tulikuwa tukitumia madawa kwa wingi na gharama ilikuwa kubwa. Lakini baada ya mafunzo, tumeanza kuona faida. Tuko tayari kufundisha wenzetu jinsi ya kufuga bila dawa ili tuweze kupata faida na afya bora.”