Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewakumbusha waajiri wajibu wao wa kisheria. NSSF imesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa za wafanyakazi wasiosajiliwa, ili kufanikisha usajili na kuhakikisha michango inawasilishwa kwa wakati.
Akizungumza kwenye semina kwa waajiri wa sekta binafsi katika Mkoa wa Ubungo, Meneja wa NSSF Mkoa wa Ubungo, Joseph Fungo, amewapongeza waajiri kwa kushiriki katika shughuli hii inayolenga kutoa elimu kuhusu hifadhi ya jamii na kuwakumbusha kutimiza wajibu wao.
Fungo alisema kwamba kutoa elimu kwa wanachama na waajiri wa sekta binafsi katika Mkoa wa Ubungo kutaimarisha ushirikiano baina ya waajiri na Mfuko, na kuongeza ubora wa huduma kwa wanachama na wadau wote.
Ofisa Sheria wa NSSF, Geofrey Ngwembe, alisisitiza umuhimu wa waajiri kuifahamu sheria ya hifadhi. Alisema, "Kujua sheria hii ni wajibu wa kila mwajiri ili kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria hiyo."
Ngwembe aliongeza kuwa, kuelewa sheria na kanuni za adhabu kutasaidia waajiri kuhakikisha michango ya wanachama inawasilishwa kwa wakati, na hivyo kuepuka adhabu zisizo za lazima.
Semina hiyo ililenga kuwakumbusha waajiri juu ya majukumu yao ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kusajili wafanyakazi na kuwasilisha michango kwa wakati. Mada mbalimbali zilitolewa, ikiwa ni pamoja na matakwa ya Sheria ya Mfuko na matumizi ya mifumo ya Tehama iliyoboreshwa.