Ili kupanua wigo wa ajira na kufanya kazi nchi kavu na baharini, wahitimu kutoka vyuo vya Veta wamehamasishwa kujiunga na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).
Wahitimu wa Veta ni wale ambao wanamaliza ngazi ya Level Three na wana ufaulu wa angalau masomo mawili (D 2) katika mtihani wa kidato cha nne.
Katika maonesho ya miaka 30 ya Veta yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Mkufunzi kutoka DMI, Kapteni Emmanuel Nanyaro, alisisitiza kuwa sekta ya bahari inakua kwa kasi, na wahitimu wanaopitia chuo hicho wanaweza kufanyakazi kimataifa.
DMI inashiriki katika maonesho haya kutoa elimu kwa umma kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa na kuimarisha uhusiano kati ya DMI na Veta.
Kapteni Nanyaro alifafanua, “Watu wa Veta wanaweza kujiunga na DMI ili kupanua wigo wa ajira. Mtu mwenye level three ya Veta akija kwetu anaweza kujifunza umeme wa kwenye meli na kuchomelea melini, kwani ufundi huu ni tofauti kati ya nchi kavu na baharini. Hii itawapa uwezo wa kufanya kazi kwenye mazingira mbalimbali na kupata kipato kizuri.”
Wanafunzi wengi waliomaliza Veta kisha kujiunga na DMI wameshafaulu kufanya kazi nje ya nchi kama wachomeleaji na mafundi umeme kwenye meli.
“Tuna wito kwa vijana wanaosoma Veta kwamba wanapomaliza, wasiishie tu huko; wajiunge na Chuo cha Bahari wapate elimu ya baharini, wajifunze ufundi mitambo wa baharini na namna injini za meli zinavyofanya kazi,” alisisitiza.
Chuo cha Bahari kilianzishwa kwa Sheria Namba 22 ya Bunge mwaka 1991 kwa lengo la kutoa elimu na mafunzo ya baharini, pamoja na kufanya tafiti na ushauri elekezi kwa taasisi za umma na binafsi.