*Kuhusu Urejeshaji wa Mikopo Bila Riba*
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Kampuni Airpay Tanzania na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) katika kusaidia wananchi kurejesha mikopo ya bila riba inayotolewa na Serikali ya Zanzibar.
Ushirikiano huu unalenga kuongeza urahisi kwa wakopaji katika kurejesha na kukopa fedha kwa wakati, na unatarajiwa kuboresha mifumo ya malipo ya kifedha kidijitali. Gavana Tutuba alisema hayo katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam, kilichojumuisha wadau kutoka sekta ya fedha na benki.
“Nina furaha kuona ZEEA ikishirikiana na Airpay kuanzisha mfumo wa kidijitali utakaorahisisha urejeshaji wa mikopo ya bila riba, ili fedha hizo ziweze kuwasaidia wananchi wengine. Naamini mfumo huu utasaidia katika kurejesha pesa hizo,” alisema Tutuba.
Aliongeza kuwa watu wengi wanashindwa kurejesha mikopo, lakini mfumo wa Airpay unatarajiwa kuwasaidia wakopaji kurejesha fedha hizo kwa urahisi, hivyo kupunguza muda na usumbufu wa ziada kwenye michakato ya benki.
Tutuba alieleza kuhusu hali ya mikopo kwa Zanzibar, akisema kuwa asilimia 28 ya mikopo imekuwa ikirejeshwa ipasavyo, lakini baadhi ya wakopaji bado hawajarejesha bila sababu sahihi.
Mihayo Wilmore, kiongozi wa Mifumo kutoka Airpay Tanzania, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mteja anapata urahisi katika kurejesha mikopo. Alisema tayari kuna mipango ya kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania ili kuboresha mfumo wa kurejesha mikopo.
Kwa upande wake, Juma Burhan Mohamed, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, alisema tangu mwaka 2022, wakala wao umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 34.9, ikiwawezesha wanawake 14,000 na wanaume 9,000. Alisisitiza kuwa huduma za mtandaoni zinahitajika zaidi ili kuendelea kufikia malengo ya maendeleo ya kiuchumi.
“Wananchi wanapaswa kuelewa kuwa fedha wanazopata kutoka serikali ni kwa ajili yao wenyewe, na ni muhimu kurejesha kwa wakati ili kusaidia maendeleo ya taifa,” aliongeza Juma.
Kwa kumalizia, alitoa shukrani kwa kampuni ya Airtel na Benki ya TCB kwa ushirikiano wao katika kuimarisha mifumo ya malipo kidijitali, akisema kuwa hii ni hatua muhimu katika kujenga uchumi jumuishi visiwa vya Zanzibar.