Dar es Salaam. Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) imepata tuzo ya kimataifa kwa juhudi zake za kuboresha usalama wa barabara. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega na Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta, walipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye hafla iliyofanyika Februari 17, 2025.
Tuzo iitwayo iRAP Gary Liddle Memorial Trophy ilitolewa kutokana na mchango wa Tanroads katika mpango wa Ten Step Plan Tanzania, ambao unalenga kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara na kupunguza hatari za ajali.
Tukio la utoaji wa tuzo hiyo lilifanyika mjini Marrakech, Morocco, katika mkutano wa kimataifa wa mawaziri kuhusu usalama barabarani. Tanroads ilikuwa miongoni mwa washindani watano kutoka nchi 11, ikikabiliwa na taasisi nyingine 12 kutoka duniani kote, ikiwemo kutoka India, Australia, Peru, na Saudi Arabia.
iRAP Gary Liddle Memorial Trophy hutolewa kwa mamlaka na wakala za barabara zinazojitahidi kuondoa hatari kwenye barabara zao. Tuzo hii ni ya kudumu, ikiwa ni heshima kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya iRAP, Gary Liddle AO, aliyefariki mwaka 2023.