Na WAF – Malawi
Serikali ya Tanzania, ikishirikiana na wadau wa Sekta ya Afya, imefanya hatua kubwa katika kujenga uwezo wa kukabiliana na dharura za afya. Uwekezaji umelenga kuimarisha mifumo ya afya, ushirikiano na wadau, na kuanzisha mifumo ya tahadhari mapema pamoja na ufuatiliaji wa abiria na vyombo vya usafiri.
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, alitoa taarifa hii Februari 10, 2025, wakati wa Mkutano wa 74 wa Mawaziri wa Afya wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati, na Kusini (ECSA – HC) kuhusu mbinu za kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na masuala ya dharura za afya za umma, uliofanyika nchini Malawi.
“Magonjwa ya mlipuko yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara, yakiathiri usalama wa afya za wananchi. Serikali ya Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukabiliana na dharura za afya huku ikiongeza udhibiti dhidi ya magonjwa ya mlipuko,” alisema Waziri Mhagama.
Akiwasilisha taarifa, Waziri Mhagama alieleza kwamba mnamo Machi 2023, Tanzania ilikabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg kwa mara ya kwanza, na ilifanikiwa kudhibiti kwa chini ya miezi mitatu. Aidha, mlipuko wa pili ulitokea Januari 20, 2025, ambapo hatua za kudhibiti zilitekelezwa kwa haraka, ikionesha uwezo wa Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya magonjwa.
Waziri Mhagama pia alisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhu endelevu za uzalishaji wa huduma za chanjo, tiba, na bidhaa za matibabu ili kukabiliana na tishio la magonjwa ya milipuko. Aliongeza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Afya ya ECSA ili kuimarisha usalama wa afya wa kikanda na kimataifa, akitoa wito wa kusaidia uratibu wa Chuo cha Madaktari wa Afya ya Umma (ECSA-COPHP).
“Ushirikiano wetu wa kikanda ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa kushughulikia dharura, jambo ambalo linachangia pakubwa katika usalama wa afya ya jamii,” alisisitiza Waziri Mhagama.