MANYARA: Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amethibitisha kwamba Serikali inajitahidi kurejesha hadhi ya Tanzanite kupitia minada ya madini itakayofanyika ndani na nje ya nchi. Hii ni hatua muhimu kwa wafanyabiashara na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Mavunde alizungumza katika uzinduzi wa mnada wa madini ya vito uliofanyika leo, Desemba 14, 2024, katika Mirerani, Manyara, baada ya kuishiwa kwa minada tangu mwaka 2017.
Amesisitiza umuhimu wa kudhibiti biashara ya madini na kuzuia utoroshaji, akisema kwamba kuwepo kwa minada kutachochea uongezaji thamani wa madini ya vito.
“Madini ya vito yanafaa kwa matumizi ya kifahari, na tunapaswa kushindana kimataifa. Serikali inaendelea kuboresha hadhi ya Tanzanite ili ikashindane vyema duniani,” alisema Waziri Mavunde, akiongeza kuwa,
“Hatua ya kwanza ni kuanzisha minada ya ndani na ya kimataifa ili kuweza kuongeza thamani ya madini yetu. Tanzanite ni adimu, na tunapaswa kulinda hadhi yake ili bei yake iweze kupanda na faida ikapatikana kwa wafanyabiashara.”
Waziri Mavunde alifafanua kuwa katika vipengele vya mawe duniani, dhamani ya jiwe inaanzia kwenye Precious, semi-Precious, hadi kuwa jiwe la kawaida, na lengo ni kuhakikisha Tanzanite inabaki kuwa na hadhi ya juu.
Amesema, “Tukiacha liwe la kawaida, madini haya yatauzwa kwa gharama ndogo, na hatutakubali kuona hadhi ya Tanzanite ikishuka.”
Katika hatua nyingine, Mavunde alihakikishia wadau wa madini kuwa Serikali haitaichukua madini ya mtu baada ya mnada, na madini yatakayo baki yatakabidhiwa kwa wahusika.
Amesema, “Tumeshughulikia madini yaliyobaki kutoka mnada wa mwaka 2017, na hatutakubali hisia za watu kwamba serikali itachukua madini yao.”
Waziri aliongeza kuwa, eneo la kujenga ‘Tanzanite Exchange Centre’ tayari litajengwa Manyara, pamoja na mpango wa kuunda ‘Tanzanite Smart City’ ambayo itakuwa na hoteli na mikutano makubwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alieleza kwamba katika mnada huu, wauzaji 195 wakiwemo wafanyabiashara wa madini 120, na kiasi cha madini kilichotolewa ni kilogramu 184.06, kinachokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi bilioni 3.10.
Wakati akizungumza, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, amempongeza Waziri kwa kuwekeza katika utafiti wa madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na kueleza kuwa, kamati itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara ili kukuza mchango wa sekta ya madini kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, amepongeza jitihada za Serikali katika kuboresha uchumi na kuanzisha masoko ya madini nchini, akasisitiza umuhimu wa biashara ya madini ya vito kuendelea kufanyika Mirerani.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, aliongeza kuwa minada ya madini ya vito itachangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kutoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.