Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imeanzisha mpango wa mikopo kwa vijana wanaotaka kujiajiri na kujiingizia kipato masaa 24, hatua hii inaimarisha juhudi za kukabiliana na changamoto za ajira na kuhamasisha uzalishaji.
Katika uzinduzi wa mpango huo uliofanyika Soko la Kariakoo, Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila, alisisitiza kuwa serikali inahakikisha ulinzi na usalama wa wafanyabiashara na mali zao.
“Kwa sasa tunatekeleza ‘Dar Biashara Masaa 24’, ambapo wafanyabiashara wanapatiwa huduma muhimu kama intaneti ya bure, kamera za CCTV kwa usalama, na mazingira bora ya kufanya biashara,” alisema Chalamila.
Aliongeza kwamba serikali inafanya mazungumzo na Waziri wa TAMISEMI kuhusu kuboresha muda wa kuuza pombe ili kuhakikisha matumizi yake yanafanyika katika mazingira sahihi.
Mpango huu utaenelea katika masoko mengine kama Manzese na Mbagala, na wafanyabiashara wa Soko la Congo na maeneo mengine wanakaribishwa kushiriki.
Mpango huu una lengo la kuboresha mazingira ya biashara, kuhamasisha vijana kujiajiri, na kuchangia ustawi wa kiuchumi katika jiji la Dar es Salaam.