Katika juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea na mipango ya elimu, uhamasishaji na usambazaji wa bidhaa za Nishati Safi za Kupikia katika Mikoa yote Tanzania Bara. Lengo ni kuhakikisha kuwa 80% ya wananchi wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Haya yamezungumziwa Jijini Arusha na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi wa REA, Mhandisi Emanuel Yesaya, wakati wa maonesho kuelekea Siku ya Wanawake Duniani 2025.
“Tunaendelea kutoa elimu na kuonyesha bidhaa mbalimbali za nishati safi ya kupikia, huku tukihamasisha wananchi, hususan akina mama, kutumia nishati safi ili kuboresha maisha yao na kulinda afya zao,” alisema Mhandisi Yesaya.
Aliongeza kuwa REA imeandaa mipango mbalimbali inayolenga kumrahisishia mwanamke maisha, akizingatia kuwa yeye ndiye kinara wa jiko katika familia.
Serikali inatambua umuhimu wa kulinda afya za wananchi wake na kuhifadhi mazingira yaliyoathirika na matumizi ya nishati chafu, kama kuni na mkaa. Mwelekeo sasa ni kujikita katika matumizi ya nishati safi za kupikia ambazo zinapatikana kwa gharama nafuu kwa wananchi.
“Hii ni fursa muhimu iliyotolewa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anaongoza katika juhudi za kuboresha matumizi ya nishati safi kwa wananchi. Tunatoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa hii,” alisema Mhandisi Yesaya.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa REA, Bi Martha Chassama, alitoa wito kwa wanawake kutembelea banda la Wizara ya Nishati ili kujifunza kwa kina umuhimu wa kutumia nishati safi za kupikia.