Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ametangaza kuwa waokota taka wana mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa, wakiwa sehemu muhimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa waokota taka rejeleshi jijini Dar es Salaam, Profesa Mkumbo alisema kuwa shughuli zinazofanywa na waokota taka ni muhimu katika kukabiliana na tatizo la taka linalokabili jiji hilo na kuokowa kizazi cha sasa na kijacho.
“Naomba mkumbuke kuwa mna mchango mkubwa katika kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa safi na salama. Mnaisaidia Serikali katika kutekeleza majukumu yake, hasa katika ulinzi wa mazingira, ambao ni msingi wa Dira ya Maendeleo ya 2050,” alisema.
Pia, aliangazia changamoto ya ajira kwa vijana nchini, akisema jitihada zinazofanywa na jamii kujitafutia kipato zinapaswa kuungwa mkono na Serikali.
Katika kutafuta fursa kwa waokota taka, Profesa Kitila alisisitiza kuwa Serikali inaendelea na mazungumzo na kiwanda cha saruji Tanga kuhusu uwezekano wa kutumia nishati inayotokana na taka. Kiwanda hicho kinatarajiwa kutumia nishati hii katika uzalishaji wake, na waokota taka watakuwa miongoni mwa wateja wakubwa katika mipango hiyo.
Profesa Mkumbo pia aliahidi kushughulikia changamoto za vifaa vinavyohitajika ili waokota taka wafanye kazi zao kwa ufanisi, akitaja kuwa kundi hili tayari linatambuliwa na lina haki ya kuheshimiwa.
Wakati huo, Makamu Mwenyekiti wa umoja wa waokota taka, Said Mohamed, alieleza changamoto wanazokumbana nazo, ikiwemo malipo duni wanapokusanya taka. Aliongeza kwamba wanakabiliwa na dhihaka na kutothaminika katika jamii, hali inayopelekea baadhi yao kudhulumiwa.
Said alipendekeza kuwa Serikali iwezeshe uratibu wa vipimo vya taka na kuwasaidia waokota taka kwa huduma za bima ya afya kutokana na mazingira hatarishi wanayofanyia kazi. Ombi hilo lilitambuliwa na Profesa Kitila, akiahidi kuwa Wakala wa Vipimo utashughulikia masuala ya vipimo ili kuboresha kazi hiyo ya muhimu.