Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewataka maofisa manunuzi na wakurugenzi wa halmashauri nchini kutoa taarifa kuhusu kampuni ambazo zimeomba tenda lakini hazijatekeleza kazi ndani ya siku 28, ili kuchukuliwa hatua stahiki.
Kauli hii ilitolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, alipokuwa akizungumza na maofisa ununuzi na wakurugenzi wa halmashauri katika kikao kazi kuhusu matumizi ya mfumo wa ununuzi wa kielektroniki (Nest) jijini Dodoma.
Simba alieleza kwamba kunakuwepo na tabia ya kampuni kushinda tenda kisha kutokonekana kwenye kazi zao, hali inayosababisha halmashauri kukabiliwa na gharama za kutafuta mkandarasi mwingine na mchakato wa muda mrefu.
“Mkipata changamoto ya aina hii wasilianeni nasi ndani ya siku 28 ili tuweze kufungia kampuni hiyo kufanya kazi nchini. Mfumo wa Nest umeunganishwa na taasisi 20, ikiwemo Nida, TRA na Brela, kuhakikisha kampuni hizo haziwezi kufanya kazi nyingine nchini,” alisema Simba.
Aidha, alisema PPRA inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo baadhi ya taasisi kutotumia mfumo wa Nest kwa ununuzi wa umma kama sheria inavyoelekeza.
“Tunaendelea kutoa elimu na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya taasisi zinazokiuka taratibu hizo,” aliongeza Simba.
Simba alifafanua kwamba mfumo wa Nest umesaidia kuokoa Sh14.94 bilioni kwenye ukaguzi wa mabilioni ya fedha zilizotumika kwenye ununuzi wa umma nchini.
Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma inatoa mamlaka kuhusu kampuni zinazoshindwa kutekeleza kazi kwa mujibu wa mkataba wa manunuzi ya umma, na kampuni hiyo inaweza kuwekewa marufuku katika zabuni za umma kwa kipindi fulani.
Ofisa sheria mwandamizi wa PPRA, Deusdedith Bishweko, alisema mfumo wa Nest hauruhusu kuvunja mkataba kiholela bila kufuata taratibu zilizowekwa, tofauti na mifumo ya zamani ambayo iliruhusu mkataba kuvunjwa kwa urahisi.
“Ni lazima kufuata taratibu za kuvunja mkataba, na kila mtu ajiridhishe kama kuna sababu za msingi,” alisema Bishweko.
Bishweko aliongeza kuwa mfumo unakubali mabadiliko ya bei za bidhaa, hivyo mkandarasi anaweza kulipwa gharama zilizozidi kwenye makubaliano mara wataalamu wanapojiridhisha na mabadiliko hayo.
Alisisitiza kuwa mfumo huu ni rahisi kutumia, kwani hata mtumiaji akiwa safarini anaweza kuingia kwenye mfumo na kuthibitisha tenda au malipo bila kuwa ofisini.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo, Zubeda Mbaga, aliiomba PPRA kutembelea halmashauri zenye matumizi duni ya mfumo, ili kutoa mafunzo ya kina kwa wataalamu wa ununuzi na kuboresha mchakato huo.