Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemhukumu mfanyabiashara Khamis Luwonga adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe, Naomi Marijani, na kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.
Hukumu hiyo ilitolewa leo, Februari 26, 2025, na Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu, alipokutana na ushahidi uliotolewa mahakamani. Jaji Mwanga alitaja kuwa upande wa mashitaka umethibitisha kuwa mshtakiwa alimuua mkewe kwa makusudi bila kuacha shaka yoyote.
“Tukio la mauaji lilikuwa lenye ushahidi mzito. Baada ya kutekeleza mauaji, mshtakiwa alimfunga marehemu kwenye shuka mbili na kumpeleka kwenye banda la kuku alikokuwa amechimba shimo,” amesema Jaji Mwanga.
Jaji aliongeza kuwa mshtakiwa alitumia magunia mawili ya mkaa kumchoma mwili wa Naomi, akihakikisha kila kitu kinakandamizwa na mabaki yanazikwa shambani kwake. “Kitendo hiki ni cha kutisha na hakina uhalali wowote,” alisema Jaji Mwanga.
Upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, umeomba mabaki ya mwili wa Naomi yakabidhiwe kwa familia ili wafanye mazishi, akiliambia mahakama kuwa marehemu hakupewa haki ya maziko.
Wakili wa mshtakiwa, Precious Hassan, alisema wanakusudia kukata rufaa ili kutafuta haki zaidi katika mahakama za juu.
Baba mdogo wa marehemu, Robert Marijani, alisema wameridhika na hukumu hiyo na wanangoja mabaki ya mwili wa mtoto wao ili kuweza kufanya maziko. Luwonga alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Julai 30, 2019, akishtakiwa kwa mauaji ya mkewe katika eneo la Gezaulole, Kigamboni.