Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuachana na tabia ya kuwakwamisha wananchi wanaohitaji mikopo inayotolewa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Mtaa wa Kisiwani Kata ya Bonyokwa, Mpogolo alitangaza kwamba halmashauri hiyo imetenga Sh bilioni 15 kwa ajili ya kukopesha wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Amesema baadhi ya watumishi wamekuwa wakitengeneza mazingira magumu kwa waombaji wa mikopo, hali inayosababisha kufeli kwa juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha hali ya kiuchumi kwa wananchi.
“Kuna watumishi ambao hawamuogopi Mungu, vikundi vinapokwenda kuomba msaada wanapaswa kutafuta mikataba au katiba ambazo zinatozwa fedha kati ya Sh 150,000 hadi 200,000,” alisema Mpogolo.
“Tunapewa mishahara ili kuwasaidia wananchi kupata mikopo. Tumefundishwa namna ya kuwasaidia wengine kuingia kwenye mfumo, hiyo ni jukumu letu,” aliongeza.
Mpogolo alisisitiza umuhimu wa watendaji kutoshiriki katika kuunda mkwamo wowote ambao utavuruga mchakato wa kupata fedha hizo, akisisitiza kuwa Rais ameleta fedha kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
Aidha, aliwataka wenyeviti wa Serikali za Mitaa kutumia ofisi zao ipasavyo katika kutatua changamoto za wananchi na kujenga mahusiano mazuri.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisiwani, Sulela Logeko, aliwahamasisha wananchi, haswa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, kujitokeza na kuomba mikopo hiyo ili kuboresha hali zao za kiuchumi.
Logeko pia alitangaza mpango wa kutatua changamoto za ulinzi na usalama baada ya kuongezeka kwa matukio ya uvunjaji wa amani, hususan nyakati za alfajiri.
Mwenyekiti huyo, ambaye alichaguliwa Novemba mwaka jana, alisoma ripoti ya mapato na matumizi, akiwanasihi wananchi kuhudhuria vikao vya maendeleo na kushiriki katika shughuli za mtaa.
Pia, Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo, alifafanua kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, akisisitiza kuwa bajeti ya mwaka 2025/2026 imetenga Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya na Sh milioni 70 kwa ajili ya uendelezaji wa kituo cha polisi.
Maalumu barabara ya Segerea – Bonyokwa yenye urefu wa mita 700 tayari imeshapata mkandarasi, huku barabara nyingine zikitekelezwa kupitia mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP 2), ambapo mitaa ya Msingwa, Kisiwani, na Bonyokwa itanufaika.