Dar es Salaam. Ofisa wa Bima, Said Salum Nyampanguta (29), amekutana na kesi mbili za kujipatia zaidi ya Sh38 milioni kwa njia ya udanganyifu katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo.
Anatarajiwa kujibu mashitaka yanayodai kuwa alijipatia fedha hizo kutoka kwa watu wawili tofauti kwa madai ya kuwapangisha nyumba kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), licha ya kuwa hana mamlaka ya kufanya hivyo.
Nyampanguta alifikishwa mahakamani leo, Januari 8, 2025, ambapo mashtaka yake yalifunguliwa na karani wa mahakama.
Katika kesi ya kwanza, anadaiwa Mei 11, 2024, alijipatia Sh23 milioni kupitia akaunti yake ya CRDB kutoka kwa Hamis Sebulungo kwa lengo la kumwapisha nyumba yenye Plot namba 714/11 ya Shirika la Nyumba la Taifa iliyoko Mtaa wa Jamhuri na Mkwepu.
Inasemekana baada ya kupata fedha hizo, alikataa kutekeleza makubaliano na Hamisi na kutoweka na fedha hizo, jambo linalodaiwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Katika kesi ya pili, inasemekana kuwa Mei 6, 2024, Nyampanguta alijipatia Sh15 milioni kutoka kwa Ulysious Athanas kwa lengo hilohilo la kumwapisha nyumba. Baada ya kupokea fedha hizo, anadaiwa kutosimamia makubaliano na alitoweka na fedha hizo hadi alipokamatwa.
Mshtakiwa amekataa mashitaka na kuomba dhamana. Hakimu Odoyo alitoa masharti ya dhamana, akimtaka kuwa na wadhamini wawili wenye nyaraka za utambulisho ambao wataweza kusaini bondi ya Sh30 milioni kila mmoja kwa kesi hizo mbili. Wadhamini hao wanatakiwa pia kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sawa au kutoa fedha taslimu.
Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na amerudishwa rumande, akisubiri kuwasilishwa tena mahakamani Januari 13, 2025.