Mbeya: Wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati mkoani Mbeya wameanzisha Umoja wa Jamii ya Masai (Memasa), ukilenga kupambana na mila potofu na kuhamasisha elimu miongoni mwa jamii hiyo.
Wanafunzi hao wamesema umoja huu utakuwa jibu la changamoto zinazokwamisha haki ya elimu kwa vijana, badala ya kuendelea na ndoa za utotoni au shughuli za kilimo na ufugaji kama njia pekee za maisha.
Mwenyekiti wa Memasa, Mkapa Laizer, amesema jamii ya Kimasai kwa muda mrefu imepuuzilia mbali umuhimu wa elimu, hali inayopelekea changamoto nyingi za kimaendeleo.
Kupitia Memasa, wanafunzi wanaamini watashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya mila potofu zinazozuia maendeleo ya elimu. “Tunawakaribisha wanafunzi wapya kwenye umoja huu, ambapo pamoja na sherehe, tunafanya majadiliano ya kuhamasisha kila mmoja kuwa balozi wa kueneza ujumbe wa umuhimu wa elimu kwa wazazi na walezi,” amesema Laizer.
Amesisitiza kuwa mila za kuona mtoto wa kike kama mtu wa kuolewa au kufanya shughuli za kuzalisha hazipaswi kuwa kizuizi, bali mtoto anapaswa kupata haki ya elimu ili aweze kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na kujitambua.
Asnath Almas, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, ameeleza matarajio yao kuwa umoja huu utaleta mabadiliko makubwa, hasa kwa watoto wa kike ambao mara nyingi huwa wahanga wa mila kandamizi. “Tamaduni potofu kama ukeketaji zinapaswa kufutwa, na kupitia Memasa, tunatarajia kuona usawa wa kijinsia katika jamii yetu,” amesema Asnath.
Yolita Ayoub, mwanachama wa Memasa, amesisitiza umuhimu wa mshikamano katika kufanikisha malengo ya umoja wao. “Mila potofu zitaondoka iwapo tutashirikiana na kuimarisha umoja huu. Ni lazima tubadilike na kwenda sambamba na wakati kwa ajili ya kujenga Taifa imara,” amesema Yolita.