Papa Francis Aendelea Kutibiwa Hospitalini kwa Hali ya ‘Mahututi’
Roma. Taarifa kutoka Vatican zimeonyesha kuwa Papa Francis, ambaye amekuwa hospitalini kwa zaidi ya wiki moja, bado yuko katika hali ya “mahututi” huku akipambana na changamoto za upumuaji, ikiwemo pumu.
Vatican ilieleza kuwa, “Asubuhi ya jana, Papa Francis alipata changamoto kubwa ya kupumua ambayo ilihitaji matumizi ya oksijeni kwa kiwango cha juu.” Hali hii inaripotiwa wakati Papa huyo akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma.
Hata hivyo, taarifa imeeleza kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki alikuwa macho na aliweza kutumia kiti cha kusukumwa, ingawa alidai kuandamwa na maumivu makali mwilini mwake kuanzia Ijumaa.
Kulingana na taarifa hiyo, Papa Francis pia aliongezewa damu ili kusaidia kutibu tatizo la anemia. Jumamosi, Vatican ilithibitisha kuwa kiongozi huyo atabaki hospitalini baada ya kugunduliwa na nimonia, hali ambayo itamzuia kuongoza sala ya kila wiki ya Angelus – jambo ambalo limetokea mara ya tatu tu katika kipindi cha miaka 12 ya huduma yake kama Papa.
Hali ya Papa ilionekana kuimarika mapema wiki hii, ambapo Vatican ilisema alikuwa akionyesha matumaini katika matibabu yake. Daktari Sergio Alfieri, ambaye alihusika na upasuaji wa Papa, alieleza, “Je, Papa yuko nje ya hatari? Hapana. Milango yote miwili iko wazi. Je, yuko kwenye hatari ya kifo cha ghafla? Hapana. Tiba inahitaji muda.”
Papa Francis alilazwa hospitalini Februari 14 na awali alifanyiwa vipimo vya maambukizi kwenye njia ya upumuaji, na baadae aligunduliwa na nimonia katika mapafu yote mawili.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 86 ana historia ya matatizo ya kupumua, na akiwa kijana aliugua nimonia kali iliyosababisha kuondolewa kwa sehemu ya pafu lake moja. Katika mwaka 2021, alifanyiwa upasuaji wa kuondoa sehemu ya utumbo mpana kutokana na ugonjwa wa Diverticulitis.
Aidha, Papa Francis alilazwa hospitalini mwaka 2023 kutokana na bronchitis, na hivi karibuni alikumbwa na ajali mbili zinazohusisha majeraha ya kidevu na mkono.
Huu ni muda mrefu zaidi kwa Papa kutumia hospitali tangu alipochaguliwa kuwa Papa. Ingawa madaktari wake wamemshauri kupumzika, Papa anaendelea na baadhi ya majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na viongozi wa Kanisa.
Mapema mwezi huu, Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, alimtembelea Papa kwa dakika 20 na alisema, “Tulitania kama kawaida. Hajapoteza ucheshi wake wa kawaida.”
Waumini kutoka Italia na Argentina wanaendelea kuungana kwa sala na kutunguza mishumaa ili kumuombea kiongozi wao apate afueni. “Daima tunamweka katika nia zetu,” alisema mmoja wa waumini, akiongeza kuwa wanaendelea kumweka katika sala zao.