Dar es Salaam. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imetangaza kufikia hatua ya kukifungia kituo cha televisheni cha Al Jazeera kufuatia ripoti iliyoonyesha mahojiano na kiongozi wa waasi wa M23, Bertrand Bisimwa.
Msemaji wa serikali ya DRC, Patrick Muyaya, alifafanua kwamba kibali cha matangazo kwa Al Jazeera kimeondolewa kutokana na kukiukwa kwa taratibu. Al Jazeera ilirusha mahojiano hayo katika kipindi ambacho kundi hilo la waasi linaendelea kuchukua udhibiti wa maeneo kadhaa mashariki mwa DRC.
Muyaya alisisitiza kuwa Al Jazeera ilifanya matangazo hayo bila kibali maalumu, akielezea hatua hiyo kama ukiukaji wa sheria. Wakati wa mahojiano, Bisimwa alishutumu serikali ya DRC kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Agosti.
Baada ya mahojiano hayo, uamuzi wa kukifunga kituo hicho ulitangazwa, huku Waziri wa Sheria wa Congo, Constant Mutamba, akitahadharisha waandishi wa habari kuwa watakabiliwa na hatua za kisheria watakapojaribu kuripoti kuhusu shughuli za jeshi la Rwanda na waasi wa M23.
Mashariki mwa DRC kumekuwa na mizozo ya muda mrefu kati ya serikali na waasi, ambapo kuna tuhuma kwamba Rwanda inawasaidia waasi hao. Hata hivyo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amekuwa akikanusha madai hayo, akisisitiza kwamba waasi wanaopigana hawatoki katika nchi yake.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mashambulizi mapya ya M23 katika eneo la Masisi, Kivu Kaskazini, yamesababisha idadi kubwa ya watu kukimbia makazi yao, huku zaidi ya watu 100,000 wakilazimika kuhama kutokana na mapigano yanayoendelea.