Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amethibitisha kuwa Serikali itafanya maboresho zaidi katika mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuimarisha sifa ya Tanzania kama eneo salama la uwekezaji.
Majaliwa aliyasema hayo leo, Aprili 3, 2025, wakati wa uzinduzi wa Maandalizi ya Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini (MKUMBI II) uliofanywa katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Amesema kupitia mpango huu, Serikali itajitahidi kushughulikia mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, na kiteknolojia, ikiwa ni pamoja na kuunda mazingira bora kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
“Tunaahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa wadau wote ili kufanikisha malengo ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara. Tunaamini mpango huu utaleta tija kubwa kwa Taifa letu na kusaidia katika kufikia malengo yetu ya kuwa na uchumi wa kati ulio endelevu,” alisema Majaliwa.
Akiweka wazi umuhimu wa MKUMBI II, Waziri Mkuu alisisitiza kwamba mpango huu utaongeza uvutio kwa wawekezaji wa ndani na nje, kuimarisha fursa za ajira, kuboresha miundombinu, na kufungua soko la kimataifa kwa bidhaa za ndani.
Pia, Majaliwa aliagiza kamati ya maandalizi ya MKUMBI II iharakishe hatua za kuanzisha mpango huo ili iweze kuanza kutekelezwa mara moja, huku akisisitiza umuhimu wa mazingira bora kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
Waziri Mkuu alizitaka Taasisi na Mamlaka za Udhibiti za Serikali zinazohusika na utafiti na tathmini kutoa ushirikiano wa dhati ili kamati iweze kuandaa mapendekezo yanayoshirikisha malengo mapana ya taifa yanayolingana na Dira ya Taifa 2050.
Kutokana na juhudi hizi, Waziri Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, aliongeza kuwa Serikali inatarajia kuifanya Tanzania kuwa kivutio bora kwa biashara na uwekezaji. “Kazi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ni mchakato wa kudumu,” alisisitiza.