Rombo: Ajali ya Gari Yaua Watu Tisa
Sita kati ya watu tisa waliofariki kwenye ajali mbaya ya gari iliyohusisha basi la abiria na Toyota Noah katika eneo la Tarakea, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, wamefahamika, huku miili mingine mitatu ikiwa bado haijatambulika.
Taarifa kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, zinasema ajali hiyo ilitokea Alhamisi, Desemba 26, 2024, majira ya saa 9:40 jioni katika Kijiji cha Kibaoni, barabara kuu ya Moshi-Tarakea.
Kamanda Maigwa alieleza kuwa, "Majira ya saa 9:40 jioni, gari la kampuni ya Ngessere likitokea Dodoma kuelekea Tarakea, liligongana na gari dogo la abiria likitokea Tarakea kwenda Moshi, hali iliyosababisha vifo vya watu tisa waliokuwa kwenye Noah."
Waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni pamoja na Mamasita Lowasa (27) mkazi wa Kamwanga, Damarisi Kanini Mwikau (22) mkazi wa Elasti, Kenya, Peter Urio (38), Monica Mumbua (64) raia wa Kenya, Eligatanasi Kanje (30) mkazi wa Tarakea, na Hilda Leberatus (24) mkazi wa Kikelelwa.
Kamanda Maigwa aliongeza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Noah alijaribu kupita magari mengine bila kuchukua tahadhari. Miili hiyo sasa inahifadhiwa katika hospitali ya Huruma kusubiri uchunguzi na taratibu nyingine.