Dodoma, Tanzania – Wakala wa Vipimo (WMA) umewataka Watanzania kuagiza mchanga na kokoto kwa mita za ujazo, si kwa tripu ya gari. Msemaji wa WMA, Alban Kihulla, alitoa kauli hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo, akisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo katika ujenzi.
Kihulla alisema, “Wananunua mchanga ama kokoto wasinunue kwa kuagiza gari bali waseme wanaagiza kwa mita za ujazo, ambapo ujazo huo umeandikwa pembeni ya gari unapofanya agizo.” Aliongeza kuwa matumizi sahihi ya vipimo ni muhimu ili kuondoa ukatili na udanganyifu katika biashara hizo.
Amesema kumekuwa na wafanyabiashara wanaotumia mizani isiyo sahihi na wengine wakipunguza mawe ya mizani ili kujinufaisha kwa kuwapunja wateja. “Hata vitabu vya dini vinazungumzia haki kwenye vipimo,” alisema Kihulla.
Kuhusu mafanikio ya WMA katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita, Kihulla alifafanua kwamba walipanga kuhakiki vipimo 3,923,652 vinavyotumika katika sekta mbalimbali na kufanikiwa kuhakiki 3,668,149, sawa na asilimia 94 ya malengo yaliyojiwekea.
Kwa kuzingatia dhamira ya kulinda mlaji, WMA imepewa jukumu la kusimamia kisheria matumizi sahihi ya vipimo kwa kutekeleza majukumu yake ya kuhakiki vipimo vyote vinavyotumika kwenye sekta tofauti nchini.