Viongozi wa Songwe Waonywa Juu ya Migogoro ya Kijamii
Viongozi wa vitongoji, vijiji, na serikali za mitaa katika Mkoa wa Songwe wamepatiwa onyo la kutokua chanzo cha migogoro katika maeneo yao, huku ikisisitizwa kuwa watakaobainika wataondolewa katika nafasi zao. Onyo hili lilitolewa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe, wakati wa mafunzo ya matokeo ya sensa ya watu na makazi.
Katibu huyo, Silvester Mbanga, alielezea kwamba, migogoro katika vijiji mara nyingi inasababishwa na viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya, kinyume na matarajio ya wananchi. Aliweka wazi kuwa chama hakitawavumilia viongozi wanaojihusisha na uuzaji holela wa ardhi kwa faida zao binafsi.
“Viongozi mko hapa kuwatumikia wananchi, na tunatarajia muwe mfano mzuri. Hatutaridhika na vitendo vya kusababisha migogoro, ikiwa ni pamoja na kutongoza wake za watu,” alisema Mbanga, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya waliofanya makosa.
Aidha, viongozi hao wameelekezwa kwamba mafunzo waliyopokea yanapaswa kuwa mwongozo wa kuunda vipaumbele vya maendeleo yanayohitajika kwa wananchi, kulingana na matokeo ya sensa ya mwaka 2022.
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga, alifafanua kwamba mafunzo hayo yamejumuisha zaidi ya watu 1,300, ikiwa ni pamoja na wenyeviti wa vitongoji na vijiji, na lengo ni kuwajengea uwezo katika kusuluhisha migogoro.
Mwakilishi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Benedicti Mgambi, alifafanua kwamba Mkoa wa Songwe una wakazi milioni 1.34, huku wilaya ya Mbozi ikiwa na zaidi ya wananchi 500,000, na amesisitiza umuhimu wa kutumia takwimu hizo kwa maendeleo ya kiuchumi na mipango ya maendeleo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Senjelel, Joilasi Kajange, alisema kwamba mafunzo haya yatawasaidia kuondoa migogoro ya ardhi na kwamba ni dhamira yake kutumikia wananchi kwa uadilifu.