Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatekeleza mikakati ya kuwatafuta wagonjwa 864 wa Kifua Kikuu ambao bado hawajagundulika ili waanzishiwe matibabu haraka.
Katika maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Seif Mbarouk, alifafanua kuwa mwaka 2023, jiji lilikuwa na lengo la kugundua wagonjwa 16,824 lakini walifanikiwa kugundua 15,960, hivyo wakabaki na 864 ambao bado hawajapatikana.
Dk. Seif alieleza kuwa mgonjwa ambaye hajaanza matibabu anaweza kuambukiza kati ya watu 15 hadi 20 kwa mwaka, hivyo ni muhimu kwa jamii kuwahi kwenye vituo vya afya mara wanapohisi dalili za ugonjwa huo.
Takwimu za mwaka 2024 bado zinafanyiwa uchambuzi, lakini zinaonyesha kuwa kuna upungufu wa wagonjwa ikilinganishwa na mwaka 2023, jambo linalonesha ni lazima kuongeza jitihada za kuwatafuta wagonjwa na kuwapa matibabu ili kufikia malengo ya kutokomeza Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2030.
Kampeni maalumu inaendelea kuwatafuta wagonjwa waliokosa mwaka 2024, huku Dk. Seif akiwataka wananchi kutambua kwamba ugonjwa wa TB bado upo, unatibika, na matibabu yake ni bure.
Jamii inashauriwa kutembelea vituo vya afya ikiwa wanakumbwa na dalili za Kifua Kikuu kama kukohoa kwa muda mrefu, kutokwa na jasho usiku, homa za jioni, kupungua uzito, au makohozi yenye damu.
Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani, Tanzania inachangia asilimia 87 ya wagonjwa wote wa TB duniani, ikiwa ni miongoni mwa nchi 30 zenye mzigo mkubwa wa ugonjwa huu.