Iringa: Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linashikilia watuhumiwa watatu kwa tuhuma za mauaji ya Christina Nindi (56), aliyekuwa katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, aliyepigwa risasi na kufariki Novemba 12, 2024. Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Njiapanda ya Tosa, ambapo alifariki akiwa hospitalini alipokuwa anapatiwa matibabu.
Akizungumza na wanahabari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, alisema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, huku akieleza kuwa baadhi ya watuhumiwa walikamatwa na wengine kuachiliwa baada ya kuthibitishwa kuwa hawahusiki.
“Kuna baadhi ya watuhumiwa tuliachia baada ya kubainika hawakuhusika, lakini hadi sasa tuna watuhumiwa watatu bado tunawashikilia na uchunguzi dhidi yao unaendelea. Tupo hatua ya mwisho na tutatoa taarifa,” alisema Bukumbi.
Amesema kuwa matukio ya jinai yanashughulikiwa kwa uwazi, na kuwa wamejipanga ipasavyo kukabiliana na matukio yote. Aliongeza kuwa asilimia 90 ya matukio yanabaini kwa sababu ya ushirikiano mzuri baina ya polisi na jamii, na kwamba matukio ya kihalifu yamepungua.
Pia, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, alisisitiza kuwa Serikali inaendelea na uchunguzi wa mauaji hayo kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kutoka mikoa jirani, akisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwafikisha wahusika kwenye mikono ya sheria.