Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekiri kuuawa kwa wanajeshi wake wawili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akibatia mashambulizi kutoka kwa waasi wa M23 katika maeneo ya Sake na Goma.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Gaudentius Gervas Ilonda, ametoa taarifa ikieleza kuwa wanajeshi wanne walijeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyofanyika kati ya Januari 24 na 28, 2025, na kwa sasa wanapatiwa matibabu mjini Goma.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa hatua za kusafirisha miili ya marehemu pamoja na majeruhi zinaendelea kupitia Sekretarieti ya SADC. Aidha, imesisitiza kuwa vikosi vya Tanzania vilivyoko DRC viko salama, imara, na vinaendelea na majukumu yao kama ilivyoelekezwa na uongozi wa SADC.
JWTZ imekuwa ikihusika katika operesheni za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda, ikitoa mchango wake katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Lebanon, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Liberia, Msumbiji, na DRC.