Dar es Salaam. Katika juhudi za kukabiliana na upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi katika shule za Sekondari, Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) imeanza kutoa nafasi za kujitolea kwa walimu wa Fizikia na Hesabu mkoani Kagera.
Shule zinazohusika ni pamoja na Sekondari ya Kagera River, Kyerwa, na Luteni Jenerali Silas Mayunga.
Katika taarifa iliyotolewa tarehe 12 Machi 2025, ERB imethibitisha changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi na imeanzisha mpango wa STEM Support Program (SSP) ili kusaidia ufundishaji wa Fizikia, Kemia, Hesabu, na Biolojia kupitia ufadhili wa walimu wa kujitolea.
“ERB ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Ujenzi, iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Usajili wa Wahandisi Sura ya 63. Bodi hii ina jukumu la kudhibiti tasnia ya uhandisi kwa kuwasajili na kuwaendeleza kitaaluma," imesema taarifa hiyo.
Bodi pia inatambua umuhimu wa usawa wa kijinsia katika taaluma za STEM, na inahamasisha watoto wa kike kuchangia katika masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wahandisi wanawake.
Mradi huu unaratibiwa kwa ufadhili wa wadau wa maendeleo, ikiwa ni pamoja na ubalozi wa kifalme wa Norway.
Kwa wale wanaotaka kujiunga, Bodi imeweka vigezo kuwa mwalimu anahitaji kuwa na shahada ya kwanza katika masomo ya Fizikia na Hesabu, na awe tayari kufanya kazi Kagera. Waombaji watafanya usaili kabla ya kuchaguliwa kujiunga na mpango huu wa kujitolea.
Walimu waliochaguliwa watakuwa na mikataba ya kujitolea kwa kipindi cha miezi sita, na hii inaweza kuongezwa kulingana na utendaji. Pia, watapewa posho ya kujikimu, bima ya afya, nauli ya kwenda na kurudi kituoni, pamoja na nauli ya likizo.
Bodi inasema waombaji wanatakiwa kutuma maombi kupitia barua pepe kwa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, wakieleza masomo wanayoweza kufundisha na kuambatanisha nakala za vyeti vyao vya kitaaluma na uzoefu.
Kupokea maombi kumeanza tangu tarehe 14 Machi 2025 na yataendelea hadi tarehe 31 Machi 2025.