Kibaha, Mkoa wa Pwani — Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imezindua mradi wa uchimbaji visima vitano vya umwagiliaji, ambao unatarajiwa kuboresha kilimo na maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani. Mradi huu, wenye thamani ya zaidi ya Sh311 milioni, utafaidisha vijiji vya Gwata (Kibaha), Mwetemo (Chalinze), Mkupuka (Kibiti), na Mbwara (Rufiji).
Mkataba wa mradi huo umetiwa saini leo, Februari 11, 2025, katika Kijiji cha Gwata, kati ya NIRC na kampuni ya Paragon Engineering Ltd, ambayo itahusika katika uchimbaji wa visima hivyo.
Ramadhanj Lusonge, Meneja wa NIRC Mkoa wa Pwani, alieleza kuwa visima vitachimbwa kama sehemu ya Mpango wa Serikali wa Programu ya Mfumo Himilivu wa Chakula, ukiwa na lengo la kudhibiti upatikanaji wa chakula nchini.
Visima hivyo vitasaidia katika kilimo cha mbogamboga na vitachimbwa katika wilaya tano za mkoa huo. Nickson Saimon, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, alifafanua kuwa awamu ya kwanza itahusisha visima vinne vitakavyochimbwa katika Wilaya za Kibaha, Kibiti, Chalinze, na Rufiji.
Mkuu wa Wilaya alisisitiza kuwa mradi huu unatarajiwa kuchangia ukuaji wa sekta ya kilimo cha umwagiliaji, hivyo kuboresha uchumi wa mkoa na taifa. "Visima vitafungwa umeme wa solar ili kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika wakati wote, na hivyo kuwasaidia wakulima kulima kwa misimu mitatu kwa mwaka," aliongeza.
Saimon alieleza kuwa lengo la mkoa ni kufikia visima 240 ifikapo mwaka 2030, huku akitaja kuwa kwa sasa kuna visima 140. Katika awamu hii, visima 35 vitachimbwa katika wilaya saba, ambapo kila wilaya itapata visima vitano.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wanaonufaika na mradi huu kuhakikisha wanashirikiana kulinda miundombinu ili iweze kudumu na kuwa na manufaa zaidi.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC alizungumzia mipango ya kuchimba visima 1,300 mwaka huu wa fedha, ambapo visima 70 vitahudumia mikoa 16, ikiwemo Pwani. Visima vinavyobaki vitachimbwa kupitia mitambo inayonunuliwa.