Shirika la Reli Tanzania (TRC) limehimiza wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kuwa mabalozi wazuri wa usafiri wa treni ya SGR.
Hayo yameelezwa leo Januari 16, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, wakati wajumbe walipokuwa wakisafiri kwa treni hiyo kuelekea Dodoma kwa mkutano utakaofanyika Januari 18 na 19 mwaka huu.
Kadogosa amesema kwamba watu 922, wakiwemo wajumbe zaidi ya 600 kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar, Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, pamoja na wasanii, wamesafiri kwa treni hii.
Amesisitiza kwamba ujenzi wa reli hiyo unatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambapo wajumbe wanapotumia usafiri huu wanajionea maendeleo yaliyofanywa.
“Ni heshima kubwa kwetu, na pia ni fursa ya biashara. Wangeweza kutumia mabasi au ndege, lakini tunawasafirisha wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, chama kinachounda Serikali ambacho sisi ni watumishi wake,” alisema Kadogosa.
Akaongeza kuwa utekelezaji wa shughuli zao unategemea Ilani ya Uchaguzi ya CCM, na wajumbe wanapaswa kujionea matokeo ya maono wanayoyatetea, ili kuwapa nguvu ya kuzungumza kwa dhati kuhusu mafanikio yaliyopatikana.
Kadogosa pia alisisitiza kuwa wamejipanga kukabiliana na changamoto zozote zinazoweza kujitokeza katika usafiri huo, na aliwataka Watanzania kuwa walinzi wa miundombinu ya reli.
Hivi karibuni, wamepanga kutoa huduma bora zaidi kwa kuanzisha majaribio ya mabehewa 264 kati ya 1430 yanayo tarajiwa kubeba mizigo.
Tangu kuzinduliwa kwa njia za treni za umeme kati ya Dar es Salaam na Dodoma mwezi Juni mwaka jana, TRC imeweza kusafirisha abiria zaidi ya milioni 1.4.