Katika hatua muhimu, jumla ya wananchi 97 waliokubali kuhama kwa hiari kutoka Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wamewasilisha wito kwa wananchi wengine waliobaki kujiandikisha ili kupata uhuru na fursa za kuboresha maisha yao katika mazingira salama, mbali na hatari za kuishi na wanyama wakali.
Wito huu umetolewa tarehe 19 Desemba 2024 na wawakilishi wa wananchi hao, ambapo kundi la pili lenye kaya 23 na watu 97 limehamia Kijiji cha Msomera na maeneo mengine yaliochaguliwa. Kati ya waliohamia, mifugo 196 pia imehamishwa kwa hiari.
Bw. Daudi Melubo kutoka Kijiji cha Kayapus, mojawapo ya waliohama, alieleza kuwa uhamaji huo umetokana na kukosekana kwa uhuru wa kiuchumi ndani ya hifadhi. “Nimehamia Msomera kwa sababu huko kuna uhuru wa kujiendeleza, nitajenga nyumba, nitamiliki ardhi, na watoto wangu wataenda shule bila hofu ya wanyama. Nawashauri ndugu zangu kujiandikisha na kuhama kwa hiari ili kuboresha maisha yao,” alisema Daudi.
Bi. Naishiye Sembeta aliongeza kuwa wanawake wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi, akisema, “Tumekuwa tukitembea umbali mrefu kutafuta kuni, lakini sasa tunahamia Msomera na tunaamini maisha yetu yatakuwa bora zaidi.”
Meneja wa mradi na Afisa Uhifadhi Mkuu, Flora Asey, alitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa uhamaji huo akisisitiza kuwa hadi leo, kaya 1,678 zenye watu 10,073 na mifugo 40,593 zimehamishwa kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kuelekea Msomera na maeneo mengine yaliyochaguliwa.
Assey aliongeza kuwa utaratibu wa kuandikisha na tathmini ya maendelezo unaendelea ili kuhakikisha wananchi wanaondoka kwa muda mfupi na kwa urahisi. Serikali inaendelea na zoezi hili ili kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kuishi katika maeneo salama yenye huduma za kijamii muhimu kwa maendeleo yao.