Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa ushirikiano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeanzisha mafunzo ya Soka la Ufukweni (Beach Soccer) kwa maofisa na askari ili kukuza mchezo huu nchini.
Mafunzo haya, yakiwa na washiriki 30, yanafanyika katika kambi ya Jeshi Mbweni JKT Kikosi 836 JK, jijini Dar es Salaam, na yanatarajiwa kufungwa tarehe 14 Machi 2025.
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Beach Soccer, Jaruph Rajab, amesema kuwa lengo kuu la mafunzo haya ni kuongeza wigo wa walimu na kuendeleza vipaji vya mchezo huo, ili kuunda timu imara ya Taifa.
“Walimu hawa watakuwa wajumbe katika vikosi mbalimbali na kuwatafuta wachezaji wenye talanta ya mchezo huu maeneo tofauti nchini. Mchakato wa mafunzo haya utakuwa endelevu kwani hii ni kozi ya awali na tunatarajia kuendelea na mafunzo katika maeneo mengine,” alisema Jaruph.
Mratibu wa kozi hiyo, Meja Hassan Juma kutoka Kurugenzi ya Utimamu wa Mwili, Michezo na Utamaduni Makao Makuu ya JWTZ, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya JWTZ na TFF unalenga kupeleka mchezo huo kwenye kiwango cha kimataifa.