Wajasiriamali nchini wameshauriwa kutumia Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupima bidhaa zao kabla ya kuzipeleka nje ya nchi ili kuepuka kurudishwa kwa kushindwa kutimiza vigezo.
Maabara hizo zimepata ithibati, hivyo mfanyabiashara au mjasiriamali anayezitumia atapata matokeo yanayokubalika kitaifa na kimataifa.
Ushauri huu umetolewa Machi 3, 2025, na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uchunguzi wa Bidhaa za Mazingira kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambaye alizungumza katika mahojiano kwenye maonesho ya wanawake na vijana wajasiriamali yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), ambapo mamlaka hiyo inashiriki.
Kaimu Mkurugenzi amesema, “Tuna kurugenzi maalumu kwa ajili ya uchunguzi wa bidhaa zinazozalishwa nchini. Tuna uwezo wa kuwapa taarifa ya uchunguzi ambayo imeainisha viwango, viambata, ubora na usalama wa bidhaa. Lengo ni kuhakikisha bidhaa zinazalishwa zinamlinda mlaji na zinakidhi viwango vya soko la ndani na la kimataifa.”
Amesisitiza, “Maabara yoyote ili iweze kutambulika kimataifa lazima iwe na ithibati. Ithibati ni kigezo muhimu kinachomuwezesha mfanyabiashara kuuza bidhaa nje ya nchi. Maabara zetu zimepata ithibati, hivyo mfanyabiashara anayatumia atakuwa na uwezo wa kupata matokeo yanayokubalika katika masoko ya ndani na nje.”
Aidha, amesema wanatumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu shughuli za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuhakikisha wajasiriamali wanazalisha bidhaa za viwango vya ubora vya kitaifa na kimataifa.
“Kupima sampuli zako kwa kutumia maabara ambayo ina ithibati kunakupa matokeo sahihi ambayo yanakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, na hivyo kuwa na uhakika wa bidhaa unayouza,” alisisitiza.
Ameongeza kuwa, “Watumiaji wanahitajika kuwa na uelewa wa bidhaa wanazonunua kuhakikisha kwamba zimeshuhudiwa katika maabara zinazotambulika kitaifa na kimataifa ili kuweza kupata bidhaa bora.”
Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara alitembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwenye maonesho hayo na kuipongeza kwa kazi nzuri ya uchunguzi wa sampuli mbalimbali, akitoa wito wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo.