Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amezielekeza mamlaka za maji kupunguza kiwango cha upotevu maji ili kuepusha hasara ya shilingi bilioni 114.12 iliyotokana na upotevu huo mwaka huu.
Dk. Biteko amesema hayo jijini Dar es Salaam Machi 19, 2025, wakati akizindua taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Maji kwa mwaka 2023/24. Alisisitiza kwamba upatikanaji wa huduma za maji ni haki ya msingi, hivyo ni muhimu kulinda vyanzo vya maji ili kuwezesha upatikanaji huo.
Amesema ni wajibu wa jamii kuhakikisha usafi wa mazingira, kupanda miti, na kuhifadi misitu, ili kuendelea kupata na kutumia rasilimali za maji.
“Tusipotunza vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira, tutajikuta katika mtanziko mkubwa wa maji,” alisema. Aliongeza kwamba kukosekana kwa rasilimali za maji kwa baadhi ya watu kunaweza kuwa chanzo cha migogoro na machafuko katika jamii.
Kwa sasa, asilimia 84 ya maeneo ya mijini na asilimia 79.6 ya maeneo ya vijijini zimeunganishwa na huduma ya maji, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7 kutoka kipindi cha mwaka uliotangulia.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, aliongeza kwamba kumekuwa na ongezeko la ubora wa viwango vya maji na udhibiti wa upotevu wa maji, ambao unasababisha hasara kubwa, hasa unapothamanishwa kifedha.
Amesifu EWURA kwa kazi nzuri na kutoa taarifa inayoonyesha hali halisi, akisema mamlaka zinazofanya vizuri zinapata tuzo kama motisha ya ushindani wa kimaendeleo.
Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Profesa Mark Mwandosya, alitia mkazo kwenye umuhimu wa serikali kutoa kipaumbele kwa sekta ya maji, huku akionyesha kwamba bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 206 mwaka 2010/11 hadi shilingi bilioni 558 mwaka 2024/25.
Amesema uwekezaji katika sekta ya maji unaleta faida zaidi ya mara saba ya mtaji, ambapo uwekezaji wa dola 1 unaweza kuleta faida ya dola 7 katika uchumi wa taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andelile, alisisitiza kwamba licha ya mafanikio yaliyofikiwa, bado kuna changamoto kadhaa zinazotokana na utegemezi wa mamlaka za maji kwa serikali.
Changamoto nyingine ni uchakavu wa miundombinu ya maji inayosababisha upotevu wa maji na hasara kwa serikali. Mamlaka za maji zilizofanya vizuri katika udhibiti wa upotevu wa maji ni Maganzo 4%, Nzega 6%, Kashuwasa 11%, Biharamulo 12% na Mwanuzi 13%. Mamlaka zilizoshindwa kudhibiti upotevu huo ni Rombo 70%, Handeni 69%, Mugango/Kyabakari 68%, Ifakara 56% na Kilindoni 55%.