Kwa siku mbili mfululizo, Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa 19 wa Shirikisho la Wadau wa Korosho Afrika (ACA) utakaofanyika Novemba 18 na 19, 2025 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julias Nyerere.
Mkutano huo utaambatana na maonyesho ya bidhaa na teknolojia za uzalishaji na usindikaji wa korosho, na utawakutanisha wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa zao hilo kutoka ndani na nje ya Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, amesema mkutano huu unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 500 kutoka nchi 30 barani Afrika. Lengo la mkutano huu ni kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya korosho, huku kauli mbiu yake ikiwa “Korosho kwa Ukuaji wa Uchumi Endelevu.”
Alfred alisema, “Mkutano huu ni jukwaa muhimu kwa wadau wa sekta ya kilimo cha korosho kujadili changamoto na fursa za uwekezaji, pamoja na njia bora za kuboresha sekta hiyo. Serikali ya Tanzania imeweka mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya korosho ili kuongeza uzalishaji na kuchochea ajira kwa vijana.”
Mkurugenzi wa Jukwaa la Korosho Afrika (ACA), Ernest Mintah, alieleza kuwa mkutano huu ni fursa kubwa kwa Tanzania kujifunza kutoka kwa nchi zilizoendelea, kama Ivory Coast, ambayo imepiga hatua kubwa katika uzalishaji na usindikaji wa korosho. “Mkutano huu utakuwa jukwaa muhimu kwa wakulima, wawekezaji, na wadau wa kilimo cha korosho kujadili mbinu bora za kuimarisha sekta hii,” alisema Mintah.
Ameongeza kuwa, takwimu zinaonyesha kwamba Afrika ina zaidi ya hekta 600,000 za ardhi inayoafaa kwa kilimo ambacho hakitumiki, hivyo ni muhimu kuhamasisha uwekezaji ili vijana wahamasishe fursa zilizopo kwenye kilimo na kutekeleza matumizi bora ya ardhi hiyo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wabanguaji wa Korosho Tanzania (TACP), Bahati Mayoma, amesema mkutano huu utaanzisha mjadala wa kina kuhusu masuala ya uzalishaji, ubanguaji, rasilimali watu, na masoko ya kimataifa ya korosho.
Tanzania inazalisha korosho bora duniani ikiwa ya nne Afrika, inayotumia wastani wa hekta 300,000, sawa na asilimia mbili ya eneo zima lililonalo, lakini kiasi kikubwa kinasafirishwa nje ya nchi, hivyo kutoa ajira huko na kupunguza uchumi wa ndani.