Mafanikio ya TANROADS Katika Uongozi wa Rais Samia Suluhu
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetangaza mafanikio makubwa katika miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usafikaji wa barabara kuu na za mikoa wakati wote wa mwaka kupitia matengenezo ya mara kwa mara.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Miundombinu na Mipango wa TANROADS, Ephatar Mlavi, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetekeleza miradi mingi yenye viwango vya juu, ambayo imeimarisha miundombinu ya usafiri nchini.
Kati ya mafanikio hayo, mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) umefikia hatua muhimu, ambapo awamu ya pili yenye urefu wa kilometa 20.3 imekamilika. Barabara zinazohusiana zinajumuisha Mbagala – Mzunguko wa Bandari (Bendera Tatu), Bendera Tatu – Kariakoo, Sokoine – Zanaki, na Kawawa – Morogoro (Magomeni). Awamu ya tatu ya mradi huo, inayoelekea kutoka katikati ya jiji hadi Gongo la Mboto (km 23.3), imefikia asilimia 74 ya utekelezaji.
Kwa upande mwingine, TANROADS inatekeleza ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Dodoma (Outer Ring Road) yenye urefu wa kilometa 112, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji. Hadi Februari 2025, sehemu ya kwanza (km 52.3) imekamilika kwa asilimia 91, wakati sehemu ya pili (km 62) ikiwa imefikia asilimia 85.
Miradi mingine inayofadhiliwa na benki mbalimbali ni pamoja na upanuzi wa barabara zinazoingia na kutoka Dodoma kupitia mradi wa Dodoma Integrated and Sustainable Transport (DIST), ambayo inajumuisha barabara za Chamwino (km 32), Mkonze (km 4.5), na Zamahero (km 8.5).
Katika Jiji la Mbeya, barabara kuu ya TANZAM (Uyole – Ifisi – Songwe Airport) yenye urefu wa kilometa 36 inaendelea kupanuliwa kutoka njia mbili hadi nne kutokana na msongamano, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 22. Pia, upanuzi wa barabara ya Mwanza – Usagara – JPM Bridge (km 37) unaendelea ili kuboresha mtandao wa usafiri mkoani humo.
Mkurugenzi Mlavi aliongeza kuwa TANROADS imeanzisha mkakati wa miaka mitano wa kukuza ushiriki wa wakandarasi wazawa katika miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja, kwa kutenga zabuni maalum kila mwaka wa fedha. Aidha, wakandarasi wa ndani wanaendelea kushiriki katika zabuni za ununuzi wa vifaa na ushauri elekezi, huku kiwango cha zabuni zinazotangazwa kitaifa kikiwa kimeongezwa hadi Sh bilioni 50 ili kuwanufaisha wazawa.