Dodoma
Serikali ya Tanzania imeeleza kushangazwa na uamuzi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) wa kuufungia Uwanja wa Benjamin Mkapa, licha ya kufanyiwa maboresho makubwa na kuwa tayari kwa mashindano ya kimataifa.
CAF ilitangaza kufungiwa kwa uwanja huo, ikidai kuwa haukidhi viwango vya ubora, hasa eneo la kuchezea (pitch). Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepewa jukumu la kutafuta uwanja mbadala kwa ajili ya mchezo wa robo fainali wa Kombe la Shirikisho kati ya Simba SC na Al Masri, unaotarajiwa kufanyika tarehe 9 Aprili 2025. TFF tayari limependekeza Uwanja wa Amahoro, Rwanda kama uwanja mbadala.
Katika taarifa iliyotolewa Machi 12, 2025, jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema wametokea kushangazwa na taarifa ya CAF kwani marekebisho muhimu yaliyohitajika yalishafanyika na uwanja uko tayari kwa matumizi.
“Ukaguzi wa CAF ulishafanywa wiki mbili au tatu zilizopita baada ya mechi ya Simba na Azam. Tumewasiliana na TFF na kuwapa maagizo ya kuwasilisha ombi kwa CAF waje kufanya ukaguzi mwingine hivi karibuni, kwani uwanja umefanyiwa maboresho na uko tayari kwa michuano ya kimataifa,” alisema Msigwa.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na TFF kuhakikisha uwanja huo unabaki katika orodha ya sehemu za mashindano ya kimataifa na inatoa mwito kwa CAF kuja kufanya ukaguzi mpya kabla ya kutekeleza uamuzi wa kufungia.