Serikali ya awamu ya Sita inaendelea kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii nchini, ikiwemo huduma za uhamiaji, ili kuharakisha maendeleo ya wananchi. Haya yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la Uhamiaji katika Wilaya ya Micheweni, Pemba, kuadhimisha Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Biteko alisisitiza umuhimu wa maendeleo yaliyofikiwa katika kipindi hicho, akieleza kuwa miradi mingi inaendelea kutekelezwa, na kwamba Wazanzibari wana sababu ya kujivunia. Alisema, “Serikali zote zinajitahidi kuwaletea maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, makubwa yanayotokana na viongozi wetu wa awali.”
Aliendelea kusema kuwa ujenzi wa ofisi na makaazi ya watumishi wa Idara ya Uhamiaji ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Khatib, alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kuboresha demokrasia. Aliongeza kuwa ni muhimu kwa wananchi kujua na kufahamiana ili kulinda usalama wa nchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma, alieleza kuwa maboresho yanayoendelea katika Wilaya ya Micheweni yamepunguza umasikini, huku akiahidi kuimarisha miundombinu ya barabara na maji ili kuongeza ajira na kukuza uchumi.
Ametaka Idara ya Uhamiaji kutafuta viwanja tofauti vya makazi kwa watumishi ili kulinda faragha yao. Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa kuboresha masilahi na mazingira ya kazi kwa maafisa uhamiaji katika kipindi hicho.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, alihakikishia umma kuwa Serikali itafanya kila liwezekanalo ili kuboresha mazingira ya kazi na utumishi wa Idara ya Uhamiaji, ili kuhakikisha huduma kwa wateja zinaboreka.