Dar es Salaam, Tanzania – Mwenyekiti wa Mama Ongea na Mwanao, Steve Mengele, amepongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mafanikio makubwa kwenye sekta ya utalii, ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya watalii hadi milioni 5.3, hatua ambayo imeongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa.
Steve alitoa pongezi hizo Januari 31, 2025, katika hafla maalum ya kusherehekea mafanikio ya Tanzania katika utalii iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Alisisitiza kwamba juhudi za serikali zimekuwa chachu katika kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi.
“Tunatoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya utalii. Pia, tunampongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ubunifu wao unaoudhihirishwa na kuongezeka kwa pato la Taifa kupitia utalii,” alisema Mengele.
Alimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Hassan Abbas, kwa juhudi zake katika kuwavutia watalii na kufanikisha ukuaji wa utalii wa ndani.
“Kama Mama Ongea na Mwanao, tunajitolea kushirikiana na wizara katika kutangaza, kulinda, na kudumisha utalii wa ndani kwa maendeleo ya Taifa,” aliongeza.
Steve alihitimisha kwa kuwataka wadau wote wa utalii kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa kivutio muhimu cha watalii duniani.