Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini Ethiopia kuanzia Februari 15 hadi 16, ambapo pia atashiriki katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, mkutano huo utakuwa na lengo la kumchagua mwenyekiti mpya wa AU.
“Rais Samia atashiriki mkutano wa kawaida wa 38 wa wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika,” inasema taarifa hiyo.
Mkutano huo unatarajiwa kuchagua mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2025, ambaye atachukua nafasi ya mwenyekiti wa sasa kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania.
Aidha, mkutano huo pia utachagua viongozi wapya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, ikiwa ni pamoja na mwenyekiti, makamu mwenyekiti, na makamishna sita.
Mkutano utajadili pia masuala muhimu kama taarifa ya ushiriki wa Umoja wa Afrika kwenye Mkutano wa Nchi Tajiri Duniani (G20), utekelezaji wa ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika, pamoja na taarifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Zaidi, utajadili ajenda kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, iliyopendekezwa na Tanzania. Kabla ya mkutano wa 38, Rais Samia atashiriki mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika utakaofanyika Februari 14, 2025.