Watanzania wapatao 25 wanapandikizwa betri ya moyo kila mwezi, sawa na karibu watu 300 mwaka mzima, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka watu 150 waliopandikizwa mwaka 2015/16. Katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wagonjwa wapatao 400 hadi 500 hufika kliniki ya wagonjwa wa nje (OPD) kila siku.
Betri ya moyo, ambayo pia inajulikana kama pacemaker, ni kifaa maalumu kinachosaidia kurekebisha mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida. Kifaa hiki hufanya kazi kama jenereta, kikirejesha mfumo wa umeme wa moyo ili kuhakikisha unafanya kazi kwa mpangilio sahihi. Kulingana na takwimu za kimataifa, kuna zaidi ya milioni tatu wanaoishi na betri hizo duniani, huku betri 600,000 zikipandikizwa kila mwaka.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo katika JKCI, Dk Khuzeima Khanbhai, anatanabahisha kuwa sababu inayomfanya mtu awekewe betri ya moyo ni pale mapigo yanapokuwa chini na hayako kwenye mwelekeo unaohitajika. Anasema, “Mapigo ya moyo ya kawaida yanapaswa kuwa kati ya 60 na 100. Ikiwa yapo chini na hayako katika mwelekeo sahihi, basi mtu anawekewa kifaa hicho ili kuyanawisha.”
Dk Khanbhai anaeleza kuwa kuna jenereta tatu zenye kazi ya kufanya mapigo ya moyo yaende sambamba, na tatizo lolote kwenye jenereta hizo linaweza kusababisha nyoyo kukosa mpangilio mzuri. Betri hii inakuja kuokoa hali hiyo kwa kurejesha mapigo kuwa sahihi hadi kufikia 60.
Sababu za mapigo kuwa chini ni nyingi, ikiwa ni pamoja na uvimbe katikati ya moyo au shinikizo la damu kwa wazee. Dalili za mtu mwenye shida inayohitaji betri ni pamoja na kizunguzungu, kudondoka, kuchoka, na pumzi kubana. Dk Khanbhai anabainisha kuwa maisha ya mtu anayewekewa betri hayabadiliki sana, isipokuwa lazima ajihadhari na maeneo yenye sumaku yanayoweza kuingilia mfumo wa betri hiyo.
Betri hii huwekwa mwilini kupitia upasuaji mdogo bila ya dawa za usingizi, na mara nyingi hushikilia kazi hiyo kwa muda wa miaka tisa hadi 10. Takwimu za wagonjwa zinatarajiwa kuongezeka kutokana na uelewa mkubwa wa magonjwa ya moyo miongoni mwa jamii. Dk Khanbhai anasisitiza kuwa matibabu ya betri ya moyo yanawezekana kwa gharama nafuu.