Mogadishu. Kundi la Al Shabab nchini Somalia limekiri kuhusika kwenye shambulio la bomu lililomlenga Rais wa nchi hiyo, Hassan Sheikh Mohamud.
Tukio hilo lilitokea Machi 18, 2025, ambapo wanamgambo hao walishambulia msafara wa Rais wakati wa kuelekea uwanja wa ndege wa Mogadishu.
Maofisa waandamizi wa Serikali na jeshi wamesema kuwa Rais Mohamud yuko salama baada ya shambulio hilo, huku mshauri wa Rais akithibitisha kuwa ‘yupo salama na anaendelea na safari yake’.
Wanajeshi na wakaazi wa eneo hilo walioshuhudia shambulio hilo walithibitisha kuwa msafara wa Rais ulikuwa umelengwa.
Mdau aliyejionea shambulio hilo aliona miili ya watu wanne waliouawa karibu na Ikulu. Al Shabaab ilithibitisha shambulio hilo, wakisema "Wapiganaji wetu walilenga msafara wa magari yaliyombeba Mohamud."
Ingawa Al Shabaab mara nyingi hufanya mashambulizi nchini Somalia kama sehemu ya kampeni yao ya kuipindua Serikali, shambulio hili lilikuwa la kwanza kumlenga moja kwa moja Rais Mohamud tangu 2014. Katika kipindi hicho, walishambulia hoteli aliyokuwa akihutubia.
Taarifa kutoka Wizara ya Habari ya Somalia zinasema, “Shambulizi hilo lilidhibitiwa huku Rais akiwa salama.” Kulingana na Wizara hiyo, shambulio lilitokea katika wilaya ya Xamar-Jajab jijini Mogadishu.
Sheikh Mohamud ameongoza taifa hilo kuanzia 2012 na amekuwa akifundisha katika shule na vyuo vikuu kadhaa.
Kabla ya kuwa Rais, alikuwa mwanachama wa mashirika ya kiraia na alifanya kazi nchini Somalia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Hassan Sheikh alizaliwa mwaka 1955 katika wilaya ya Jalalaqsi mkoa wa Hiraan nchini Somalia na alipata elimu yake ya msingi katika mji aliozaliwa, akihudhuria shule ya sekondari na chuo kikuu huko Mogadishu.
Aliporejea Somalia, Sheikh Mohamud alifanya kazi katika Wizara ya Elimu, akifundisha shuleni na vyuo vikuu, na pia ni mfanyabiashara aliyejiajiri.
Mnamo Agosti 2012, Hassan alikua mjumbe wa Bunge la Shirikisho na mnamo Septemba 10, 2012, alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo baada ya uchaguzi usio wa moja kwa moja.