Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesisitiza umuhimu wa kurekebisha sera kuhusu uagizaji wa magari ili kulinda viwanda vya utengenezaji wa magari nchini. Prof. Kitila alitoa kauli hiyo jana, Machi 27, 2025, wakati wa ziara yake katika kiwanda cha GF Vehicle Assemblers (GFA) kilichopo Kibaha, mkoani Pwani.
Waziri Mkumbo akiwa na viongozi wa TCI, alitembelea kiwanda hicho na kujionea mchakato mzima wa utengenezaji wa magari. Alishuhudia uzinduzi wa gari la aina ya 3400, ambalo ni la kwanza tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho.
Meneja Mkuu wa GFA, Ezra Mereng, alielezea changamoto zinazokabili viwanda vya ndani na kuwasilisha ombi la serikali kubadilisha sera na sheria za uagizaji wa magari. Alisema kuwa kampuni yao ina mpango wa kuanzisha awamu ya tatu ya upanuzi, inayotarajiwa kuleta uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 10, na kwa sasa imeajiri zaidi ya vijana 200. Katika awamu hii, wanatarajia kuajiri vijana 300 zaidi.
Ezra aliongeza kuwa, ili kufanikisha mpango huu, ni muhimu kupatikana kwa malighafi nchini, kama vile chuma na vifaa vingine. Alisema tayari wameshaanza kununua betri za magari kutoka kwa kiwanda cha ndani. “Mabadiliko ya sheria ili kulinda viwanda vya ndani ni muhimu, vinginevyo juhudi zetu zitakuwa bure. Uagizaji holela wa magari na kutokuwa na sheria za manunuzi katika miradi mikubwa ya nchi vinadhihirisha changamoto hii,” alisisitiza Ezra.