Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini limeanzisha msako wa kitaifa kumtafuta mtu anayeonekana kwenye video akidai kuwa anauza mtoto aliyembeba kwa Sh1.6 milioni.
Taarifa kutoka Makao Makuu ya Polisi, Dodoma, leo imeeleza kuwa msako huu unalenga kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha mbele ya sheria ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake.
Polisi wameeleza kuwa kitendo hiki ni cha kikatili na kinyume na sheria, na kukemea vikali tabia hiyo inayohatarisha usalama wa watoto.
Aidha, polisi wamewashukuru wananchi wanaotoa taarifa kuhusu matukio kama haya na kuwahimiza kuendelea kushirikiana na mamlaka katika kupambana na vitendo vya uhalifu.
“Jeshi la Polisi linalaani kitendo hiki na linaomba wananchi kuvikemea vitendo vya aina hii, kwani vinaweza kusababisha madhara kwa watoto. Ushirikiano wa mapema utawezesha hatua kuchukuliwa kabla madhara hayajatokea,” imesema taarifa hiyo.
Jeshi limeahidi kuendelea kushirikiana na jamii ili kuhakikisha usalama wa watoto unalindwa, na kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa wahusika wa vitendo vya aina hii.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu amekemea vikali hatua ya kijana huyo kutangaza kumuuza mtoto, akisisitiza kuwa hata polisi wamepewa jukumu la kumtafuta.
Waziri huyo amesema, “Watanzania salaam. Kijana huyu anatangaza eti tajiri apeleke Sh1.6 mil mtoto aliyembeba anazo figo 2.”
“Baadhi ya watengeneza maudhui wamefikia hatua mbaya. Nakemea vikali, tayari nimewakabidhi polisi wamtafute huyu, Watanzania tusaidiane kumjua huyu ni nani na aliko,” ameongeza Waziri huyo.