Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza kufuta matokeo ya jumla ya wanafunzi 151, ikiwa ni pamoja na 105 wa darasa la nne na 46 wa kidato cha pili, baada ya kugundulika kwa udanganyifu na matumizi ya matusi kwenye karatasi za mitihani.
Katika kauli iliyotolewa Januari 4, 2025, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed, alifafanua kuwa hatua hii imechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 na Kanuni za Mitihani za mwaka 2016.
Dk. Mohamed alisema, “Wanafunzi 100 wa darasa la nne walihusika katika udanganyifu, watano walitumia matusi, na kati yao, 98 walipata usaidizi kutoka kwa wenzao wa madarasa ya juu. Kwa kidato cha pili, wanafunzi 41 walijihusisha na udanganyifu na watano walitumia matusi.”
Pia, NECTA imechukua hatua za kufungia kituo cha mitihani cha GoodWill kilichopo Arusha, kwa kujaribu kuwasaidia wanafunzi kupata majibu kupitia chooni, kitendo kilichohusisha Mkuu wa Shule na baadhi ya walimu. Baraza limesema litapendekeza kufutwa kwa usajili wa shule hiyo kwa Kamishna wa Elimu.
Kuhusu ufaulu, Dk. Mohamed aliongeza kuwa asilimia 86.24 ya wanafunzi wa darasa la nne wamefaulu kuendelea na darasa la tano, ikilinganishwa na asilimia 83.34 mwaka 2023. Kidato cha pili, asilimia 85.41 wamefaulu kuendelea na kidato cha tatu, huku wavulana wakiwa na ufaulu wa juu zaidi (87.13%) ukilinganishwa na wasichana (83.99%).
NECTA imesisitiza kuwa hatua hizi ni muhimu kwa kudumisha uadilifu katika mitihani na kuboresha ubora wa elimu nchini.