Unguja. Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imepewa jukumu la kuandaa sheria maalumu ili kulinda nyumba mpya za makazi zinazojengwa, wakati nchi ikiendelea na juhudi za kuboresha makazi ya wananchi.
Maelekezo haya yametolewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, katika uzinduzi wa nyumba za makazi na biashara eneo la Kwa Mchina Mombasa, ambazo zimejengwa na Shirika la Nyumba Zanzibar kwa gharama ya Sh9.5 bilioni na tayari zinauzwa kwa wananchi.
Dk Mwinyi amesisitiza umuhimu wa utunzaji wa nyumba hizo, akitaka kila mteja kuwa na kamati maalumu inayohusika na utunzaji wa nyumba hizo kwa muda mrefu. “Tunajua sisi ni mabigwa wa kujenga lakini hatuna utaratibu wa kutunza, kwa hiyo wizara anzisha kamati maalumu za matunzo,” amesema Rais Mwinyi.
Aidha, amesema kuwa Serikali inatekeleza mradi wa nyumba za makazi na kuziuza kwa wananchi bila faida, lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto za nyumba zisizokuwa na viwango. “Tumeona kuna mahitaji makubwa, nyumba hapa zinajengwa lakini hazina viwango,” aliongeza.
Mpango huu unatarajiwa kukabiliana na vikwazo vilivyopo, hasa katika maeneo ya Kilimani na Michenzani, huku Dk Mwinyi akisisitiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora. “Tutahakikisha tunajenga nyumba za kisasa na kuondoa zote zilizochakaa,” alisema.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Khadija Khamis Rajab, alitoa taarifa kuhusu mradi ambao unajumuisha nyumba 82 kwa jumla ya Sh9.5 bilioni, akisema kuwa nyumba hizo zimewekewa utaratibu mzuri wa malipo na zinakaribia kuuzwa kwa wateja wote.