WACHEZAJI wapatao 122 wamejiandikisha kwa mashindano ya Lina PG Tour msimu wa pili, yanayoanza leo katika Viwanja vya gofu vya Gymkhana mkoani Morogoro.
Mashindano haya, ambayo yalianza mwaka jana, yana lengo la kumuenzi mchezaji gofu wa zamani wa timu ya Taifa ya wanawake, marehemu Lina Nkya, aliyejulikana kwa upendo wake kwa mchezo huo.
Kiongozi wa mashindano, Ayne Magombe, alieleza kuwa kati ya wachezaji 122, 47 ni wachezaji wa gofu wa kulipwa na chipukizi, huku 75 wakiwa wachezaji wasindikizaji.
Mashindano haya yatafanyika kwa siku nne na yanatarajiwa kumalizika Machi 2, 2025. Kila mwaka yanajumuisha klabu mbalimbali za wachezaji wa gofu kutoka sehemu mbalimbali nchini.
“Mashindano haya yameandaliwa na familia ya Said Nkya ili kumuenzi mama Lina. Ni muhimu wapenzi wa gofu, hasa wa Morogoro, wajitokeze kushiriki. Kwa pamoja tunaweza kukuza ujuzi na vipaji vya wachezaji wetu,” alisema Magombe.
Magombe aliongeza kuwa mashindano ya Lina PG Tour yatakuwa endelevu na wana mpango wa kuongeza mashindano zaidi kila mwaka, kutegemea na msaada wa wadau mbalimbali.
Mchezaji wa gofu wa kulipwa kutoka klabu ya Gymkhana Dar es Salaam, Fadhil Nkya, alisema kuwa kila mtu ana uwezo wa kucheza gofu na alitoa wito kwa jamii kuondoa dhana ya kwamba mchezo huu unchezwa na matajiri pekee.
“Kila mtu anaweza kucheza, na mashindano kama haya yanaweza kusaidia wachezaji kufanya mazoezi bora, ambayo yanatuwezesha kufanya vizuri katika michuano mikubwa,” alisema Fadhil.
Kwa siku nne za mashindano, wachezaji watacheza mashimo 72 kwa jumla, na mshindi lazima amalize mashimo yote kwa kiwango cha juu zaidi kuliko wenzake.
Fadhil aliongeza, “Kwa miaka mitano ijayo, gofu inatarajiwa kukua sana, na ikiwa wadau watajitokeza kutusaidia, tunaweza kufanya mambo makubwa. Tumeanza mwaka jana na matokeo mazuri yameonekana.”
Mchezaji mwingine wa kulipwa wa gofu kutoka klabu ya Gymkhana Dar es Salaam, Hassan Kadio, alisema amejitayarisha vizuri kwa mashindano na anaamini wanachezaji wa kulipwa wanapata fursa nzuri ya kujiandaa kwa mashindano ya kimataifa kupitia Lina PG Tour.
“Mashindano haya yameongeza taaluma zetu, na tunawakaribisha wachezaji wengine kujiunga na sisi kwenye mashindano haya,” alisema Kadio.