Dodoma. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilingo, Kijiji cha Msagali, Alex Chikumbi, ametoa mwito kwa Serikali na wadau kusaidia matibabu ya mgambo, Masimo Nyau, aliyejeruhiwa katika tukio la mauaji ya polisi wawili na mtuhumiwa wa unyang’anyi, Atanasio Malenda.
Katika tukio hilo lililotokea Desemba 18, 2024, askari D/Koplo Jairo Boniface Kalanda na PC Alfred John walikufa wakati D/Koplo Msuka na Nyau walipokuwa wakikabiliwa na mtuhumiwa huyo katika mapigano ya risasi.
Majeruhi walipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, ambapo Nyau alihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu zaidi.
Akizungumza Desemba 20, 2024, Chikumbi alieleza kuwa Nyau aliumia mikono yote miwili na mguu mmoja wa kushoto.
“Hospitali ya Mpwapwa waliamua kumfunga mguu hadi kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ambapo ilibidi wafanye X-Ray na kujua kuwa ni bora kuukata ili kuepusha kuoza,” alisema.
Amesema walimfanyia upasuaji usiku wa juzi ambapo walimkata mguu na kumshona mikono iliyokuwa imekatwa.
“Namshukuru Mungu anaendelea vizuri, tofauti na tulivyomleta hapa,” aliongeza Chikumbi.
Mpaka jana, Chikumbi alitumia Sh305,000 kwa ajili ya matibabu ya mgambo huyo kutoka mfukoni mwake, na sasa anaomba msaada wa kifedha kutoka kwa Serikali na watu wema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, alieleza kuwa askari hao waliuawa kwenye mapambano ya risasi na mtuhumiwa aliyedaiwa kumjeruhi na kumpora mtu Sh2 milioni.
Katabazi alithibitisha kuwa mtuhumiwa Malenda alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mapambano hayo.
D/Koplo Jairo Boniface Kalanda alisafirishwa kwenda Rukwa, huku PC Alfred John akisafirishwa kwenda Sirari, Tarime mkoani Mara kwa ajili ya mazishi.
Kabla ya kusafirishwa, miili hiyo iliagwa jana wilayani Mpwapwa ambapo Kamishna wa Utawala na Raslimali Watu, Tatu Jumbe, alilaani tukio hilo na kuhimiza jamii kutoacha kufichua tabia zisizo za kawaida miongoni mwao.
“Nawasisitiza askari wetu kuendelea kuwa waangalifu na kutumia weledi wenu mnapokuwa kazini. IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) amenituma niwaambie msikate tamaa na endeleeni kutimiza wajibu wenu kwa haki,” alisema.