Kibaha: Mchungaji wa Kanisa Anglikana la Mtakatifu Gabriel, Exavia Mpambichile, amewahamasisha waumini wake kuanza mwaka mpya na malengo thabiti, hasa katika sekta ya uchumi.
Katika ibada ya mkesha wa mwaka mpya, Mpambichile alisisitiza umuhimu wa kuwa na malengo ya kununua viwanja na kujenga nyumba za kuishi ili kuboresha maisha yao. Alionya kwamba mafanikio yanahitaji juhudi makusudi na nidhamu ya matumizi ya fedha.
"Mafanikio hayaji kwa njia ya miujiza, bali hupatikana kupitia bidii na malengo madhubuti. Lazima tuwe na nidhamu katika matumizi ya fedha tunazozipata," alisisitiza.
Aidha, aliwataka waumini kuwekeza katika biashara halali na kutumia muda wao kwa shughuli za uzalishaji mali. "Anza mwaka mpya kwa kuweka malengo. Nunua kipande kidogo cha ardhi na uanze ujenzi hatua kwa hatua. Safari ya mafanikio ni ya hatua moja baada ya nyingine," aliongeza.
Mchungaji Mpambichile pia alikazia umuhimu wa kuwa na nidhamu ya lugha na kauli njema akisema ni msingi wa mafanikio ya maisha ya kila siku. "Kauli njema huleta amani na mafanikio. Tukitumia lugha nzuri, tutavutia fadhila na kushirikiana vyema," alisema.
Katika mahubiri yake, alitoa wito kwa wazazi kuimarisha mshikamano na kuongeza upendo ndani ya familia zao ili kujenga msingi wa maadili. "Familia zenye mshikamano, umoja, upendo, na kumcha Mungu, zina uwezo wa kutatua changamoto na kufanikisha malengo yao kwa pamoja," alisema.
Waumini waliothibitisha umuhimu wa mahubiri hayo wamedai yanaelekeza njia ya kukabiliana na changamoto za maisha. "Mahubiri ya Mchungaji yametufundisha umuhimu wa kuweka malengo na kufanya kazi kwa bidii," alisema Samuel Mwegoha, mmoja wa waumini. Neema Masawe aliongeza, "Ibada hii imenifunza kuweka malengo na kuwa na nidhamu katika kila hatua ya maisha yangu."