Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeeleza sababu za kukatika kwa umeme katika treni ya mwendakosi (SGR) na kutangaza mpango wa kuanzisha mkoa maalumu wa kushughulikia changamoto za umeme zinazokabili mradi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamohanga, alitoa maelezo hayo leo katika jiji la Dodoma, akielezea mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo kuelekea miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Nyamohanga alisisitiza kuwa, mpango wao ni kuifanya SGR kuwa mkoa utakaokuwa na meneja uratibu ambaye atashughulikia mradi huo pekee pamoja na timu maalumu ya kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika.
Kuhusu kukatika kwa umeme, Nyamohanga alifafanua kuwa mradi huo unatumia laini maalumu ya umeme na changamoto ilitokana na mfumo unaotumika kwa mara ya kwanza, huku akihakikishia watanzania kuwa laini hiyo iko madhubuti na inaendelea kuimarika.
Akiangazia matatizo ya kukatika kwa umeme nchini, Mkurugenzi huyo alisema sababu kubwa ni kuzidiwa kwa gridi ya taifa kutokana na ongezeko la watumiaji wa umeme. Alitoa ahadi kwamba shirika limejipanga kuhakikisha umeme unapatikana katika kila eneo nchini.
Nyamohanga aliongeza kuwa shirika linajipanga kutumia teknolojia ya kisasa ili kurahisisha mteja kupata umeme moja kwa moja, tofauti na mfumo wa sasa wa kununua tokeni.
Kuhusu uagizaji wa umeme kutoka nje ya Tanzania, alieleza kuwa sababu kubwa ni ya kijiografia, hususan katika maeneo ya pembezoni ambapo miundombinu ni migumu. Aliashiria kuwa TANESCO ina mipango ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2027, watanzania wote, ikiwemo wale wa maeneo ya pembezoni, wanatumia umeme wa ndani.