Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amekosoa hatua ya kuruhusu magari kupita kwenye barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT) bila kibali kutoka ofisi yake.
Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mikataba ya awamu ya pili ya Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP II) hivi karibuni, Mchengerwa alisisitiza kwamba barabara hizo ziko chini ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), ambao ni sehemu ya Ofisi ya Rais Tamisemi.
“Wakati fulani mlitoa maelekezo ya kuruhusu watu kupita kwenye barabara za mwendokasi, mkasahau kuwa barabara hizo siyo za kwenu. Sasa barabara ya mwendokasi ya Mbagala imeanza kuharibika kutokana na malori makubwa yanayopita katikati. Madhara yake ni makubwa na miradi yote ya ujenzi wa barabara inaweza kuathirika,” aliongeza Waziri Mchengerwa.
Aidha, amesema Serikali itafanya mapitio ya utaratibu wa mgao wa mapato ya ndani ili kuongeza bajeti ya barabara, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa Tarura kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
“Hatuna budi kuondoa mgao wa asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya barabara. Lazima tuhakikishe Tarura ina uwezo wa kufanya kazi masaa 24 ili kuhakikisha barabara zinajengwa kwa viwango vinavyofaa na kwa muda unaohitajika,” ameongeza.
Katika hafla hiyo, Waziri Mchengerwa alishuhudia utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 84.4 katika Halmashauri mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam chini ya DMDP II.